Kiislamu vyanzo

  1. home

  2. article

  3. Uislamu Chaguo Langu 16 + Sauti

Uislamu Chaguo Langu 16 + Sauti

Rate this post

Sikiliza

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika kipindi hiki ambacho huangazia maisha ya watu ambao baada ya kufanya utafiti wa kina, wameamua kusilimu na kufuata njia iliyojaa nuru ya Uislamu. Karibuni kujiunga nami hadi mwisho wa kipindi.

@@@

Mwamko wa Kiislamu unaoshuhudiwa leo katika nchi za Kiislamu kama vile Misri, Tunisia, Yemen na Bahrain ni mifano ya kusimama wanaadamu kwa ajili ya kupinga dhulma na udikteta. Wakati thamani za Kiislamu zinapopuuzwa, udhalimu na ukosefu wa uadilifu hukita mizizi. Mazingira kama hayo ya dhulma na mbano yanaenda kinyume na fitra safi ya mwanaadamu. Kwa hivyo katika kufuata hisia ya fitra yake, mwanaadamu huamka na kutafuta njia za kuvunja minyororo ya ubaguzi na ukandamizaji na ni kwa sababu hii ndio tukashuhudua Mwamko wa Kiislamu katika nchi zilizotwa.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran chini ya uongozi wa Imam Khomeini RA yaliweza kuwafungulia watu njia ya wazi na iliyojaa nuru ya kuelekea katika saada na uhuru na hivyo kufanikiwa kulikomboa taifa kutoka minyororo ya dhulma. Ni kwa sababu hii ndio maana mara tu baada ya watu kusikia mwito wa kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wakaukumbatia Uislamu na kisha madhehebu ya Shia.

Profesa Ismail Kelbas mwanafikra wa Uhispania katika kuashiria uhai mpya wa dini katika maisha ya mwanaadamu baada ya Mapinduzi ya Kiislamu anasema: “Dini ilipata uhai, hata makanisha yakapata uhai mpya, masuala ya kidini na fikra za kidini zilianza kuangaziwa katika vyo vikuu. Ulimwengu ulianza kuelekea katika umaanawi na haya yote yalitokana na wito wa Imam Khomeini na mapinduzi yake ya kidini.”

Tokea yapate ushindi Mapinuzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979, fikra za Imam Khomeini MA zilienea kote duniani.  Fikra za Imam zilikuwa katika fremu ya Uislamu halisi wa Mtume Muhammad SAW.  Baada ya kupita muda, taathira ya fikra hizi ilibainika na leo pia, fikra za Imam zinazidi kuwavutia wanaadamu watakao ukweli katika umaanawi na kumuabudu Allah SWT.

Mehdi Casso ni Mtaliano aliyesilimu na ambaye alipata kuujua Uislamu kupitia shakhsia  tukufu ya Imam Khomeini MA.

Anafafanua zaidi kuhusu ni vipi aliikumbatia dini ya Kiislamu kwa kusema: “Tokea utotoni nilikuwa nikisikia jina la Imam Khomeini sehemu mbali mbali; lakini nilikuwa na taswira hii kuwa ni vigumu kuweza kumfikia. Baadaye nilipokuwa mkubwa, kutokana na kuvutiwa na shakhsia yake, nilijitahidi kumjua yeye na dini yake. Ni kwa msingi huu ndio utafiti wangu ukaanza na hatimaye nikafikia natija kuwa Uislamu ndiyo dini ambayo inaweza kuyaelekeza maisha yangu katika mkondo sahihi wa saada maishani.  Mimi ninaweza kusema kuwa nimeijua dini ya Kiislamu kupitia Imam Khomeini na hivyo nikaweza kuchagua dini kamili na bora zaidi.”

Suala la Umahdi na kudhihiri Imam Mahdi AJTF katika Akhiru Zaman au Zama za Mwisho ni moja kati ya masuala muhimu katika Uislamu.

Ni kwa sababu hii ndio wasomi wa kidini wakazungumzia jambo hilo kwa mitazamo mbali mbali. Suala la kudhihiri mwokozi atakayerekebisha mambo na kuleta uadilifu duniani ni kati ya masuala yanayopatikana katika maandishi ya Imam Khomeini MA.

Imam amezungumzia suala la Umahdi kwa mitazamo kadhaa kwa lengo la kuelimisha.

Mehdi Casso ametumia fikra za Imam Khomeini MA katika kubainisha itikadi ya kudhihiri mwokozi na kusema: “Imam Mahdi ATF ni dhihirisho la vyote ambavyo nilikuwa nikiwaza na kutafakari. Ananipa matumaini na nguvu. Kila wakati ninapoamka asubuhi huwa ninafikiri kuwa yamkini Imam wa Zama akadhihiri leo hii, hali hii hunipa matumaini na kunifanya niwe mwenye harakati maishani. Kwa hivyo naendeleza utafiti wa kumjua zaidi Imam Mahdi ATF. Katika Fikra za Imam Khomeini MA, vile vile Imam Mahdi ATF ametjwa kuwa mtu pekee ambaye atafanikisha malengo ya Mitume wote kuhusu Tauhidi na kwamba atakuwa mwokozi wa wanaadamu na dunia jambo ambalo lilikuwa lengo la kutumwa Mitume. Kwa mtazamo wangu, wadhifa wetu mbele ya Imamu wa Zama ni kuwa tumtumie kama wenzo wa kuujua Uislamu. Aidha tunapaswa kumjua kikamilifu Imamu wa Zama. Haya ndiyo mambo muhimu zaidi ambayo tunapaswa kuyafanya. Vile vile, tarajio langu ni kuiona dunia isiyo na dhulma na iliyojaa uadilifu. Ninataka aje aondoe maovu duniani na aje awasaidie watu wanaodhulimiwa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.”

Mehdi Casso ni kati ya wasimamizi wa Taasisi ya Imam Mahdi ATF nchini Italia. Anajitahidi sana kuhakikisha kuwa watu wengine pia wanafaidika na ubora wa dini ya Kiislamu. Mehdi Casso anafafanua hivi kuhusu shughuli zake katika Taasisi ya Imam Mahdi ATF: ‘Taasisi hii ina majukumu mawili muhimu. La kwanza ni jukumu kuhusu wanachama wa taasisi hii pamoja na Waislamu wote na jukumu la pili linahusu wasio kuwa Waislamu. Hapa tunaarifisha Uislamu kama chemichemi iliyojaa thamani za kiutamaduni na kimaanawi. Katika kufikia lengo hili taasisi imeanzisha tovuti rasmi ya intaneti yenye anwani ya www.islamshia.org kwa lugha ya Kitaliano.

@@@

Diego Rodred ni Mmarekani aliyesilimu ambaye pia aliujua Uislamu kufuatia kusoma vitabu vya Imam Khomeini MA.

Kufuatia matukio ya Septemba 11 aliamua kufanya uchunguzi zaidi kuhusu Uislamu baada ya kuona Waislamu wakituhumiwa kufuatia tukio hilo. Natija ya uchunguzi wake ilimpelekea afahamu kuwa chuki dhidi ya Uislamu ni njama inayotekelezwa kwa uongozi wa nchi za Magharibi katika hali ambayo Uislamu ni dini ya amani.

Baada ya kufanya utafiti kuhusu uadilifu na ubinaadamu katika Uislamu, Diego Rodred aliamua kuwa mfuasi wa dini ya Kiislamu miezi mitano tu baada ya tukio la Septemba 11. Akifafanua kuhusu uamuzi wake wa kusilimu anasema:  ‘Kabla ya kuchagua Uislamu kuwa dini yangu nilikuwa nimefanya utafiti wa kulinganisha fikra za Kimagharibi na za tamaduni zingine zote. Hatimaye baada ya kufanya uchunguzi niliamua kuchagua mfumo wa maisha ambao unatambua maumbile na hivyo nikachagua dini ya Kiislamu na madhehebu ya Kishia na sasa nimechagua jina la Ali Akbar.” Anaendelea kusema kuwa, katika maisha yangu ningali ninafanya utafiti kuhusu ni kwa nini tuko duniani na jinsi wazazi wanapaswa kuamiliana na watoto wao. Masuala haya yana umuhimu kwani huwa na mchango mkubwa katika kuibua shakhsia ya mwanaadamu. Baada ya matukio ya Septemba 11 Marekani, nilianza kufanya utafiti kuhusu Iran na Imam Khomeini. Nilisoma kitabu kilichoandikwa na Imam Khomeini na katika kipindi chote cha utafiti wangu kuhusu fikra za Imam niliweza kutambua umaridadi na ukweli wa dini hii tukufu. Kimsingi ni kuwa kitabu hicho cha Imam Khomeini MA ndicho kilichopelekea nisilimu.”

Kijana huyu Mwislamu Mmarekani sasa anajifunza lugha ya Kifarsi na anasema hivi: “Kutokana na kuwa Ayatullah Khomeini ndiye aliyepelekea nipate kuona nuru ya Uislamu na kutokana na kuwa Iran ni nchi yenye utamaduni na ustaarabu tajiri wenye umri wa zaidi ya miaka 5000, mimi ninajifunza lugha ya Kifarsi ili niende Iran na niweze kukutana na Waislamu wa huko kwa lengo la kuwa na uhusiano mzuri nao.”

http://kiswahili.irib.ir