Kiislamu vyanzo

  1. home

  2. article

  3. Uislamu, Chaguo Langu 3 + Sauti

Uislamu, Chaguo Langu 3 + Sauti

Rate this post

Sikiliza

Mwishoni mwa mwaka 2003, serikali ya Ufaransa ilizidisha propaganda zake chafu dhidi ya vazi la stara la Kiislamu, Hijab na madhihirisho yote ya dini ya Kiislamu nchini humo. Serikali ya Ufaransa ilitumia mbinu mbali mbali katika kuendeleza njama zake za kuchafua jina la Uislamu na Waislamu katika macho ya Wafaransa. Hii ni katika hali ambayo serikali ya Ufaransa ambayo ni ya kisekula (isiyo ya kidini) inadai kuwa kuna uhuru wa kuabudu na kwamba serikali haijihusishi na masuala ya mtu binafsi. Kwa kuzingatia misingi huo, serikali ya Ufaransa haipaswi kuwazuia raia wanawake Waislamu kuvaa hijabu.

Ingawa wakuu wa shule za Ufaransa wanasema wanatekeleza sheria za kupiga marufuku nembo na madhihirisho yote ya kidini nchini humo, lakini sheria hii kimsingi inawalenga Waislamu hasa kupiga marufuku vazi la stara la Kiislamu, Hijab. Jambo hili pekee linaonyesha kilele cha wasiwasi na hofu waliyonayo watawala wa nchi za Magharibi kufuatia kuongezeka uvaaji wa Hijabu au chochote kile kinachopelekea Uislamu kuenea katika mipaka ya Ulaya. Baada ya Ufaransa kupitisha sheria ya kupiga marufuku vazi la Hijabu katika shule na idara za serikali na vile vile kupiga marufuku kabisa uvaaji nikabu, nchi kadhaa za Ulaya zimeiga mfano huo mbaya wa Ufaransa. Pamoja na kuwepo chuki hizo dhidi ya Uislamu na Waislamu, ripoti za hivi karibuni za uchunguzi wa maoni katika vyombo vya habari vya Kimagharibi vimesema kwamba vizingiti vinavyowekwa na nchi kama vile Ufaransa na Ujerumani si tu kuwa havijaudhoofisha Uislamu bali jambo hilo limepelekea kushuhudiwa ongezeko la wanaovutiwa na Uislamu na vazi la Hijab.

Mwanamke Mjapani aliyesilimu akiwa Paris

Bi. Nakata Khaula ni mwanamke Mwislamu kutoka Japan ambaye ni mkaazi wa mji mkuu wa Ufaransa, Paris. Mjapani huyo ni kati ya waliosilimu katika miaka ya hivi karibuni na anasema kwa kuvaa Hijabu anahisi utamabulisho na thamani ya juu ndani ya nafsi yake.
Bi. Nakata Khaula anasema Hijabu ni wenzo wa ustawi na kushiriki mwanamke katika harakati za kijamii. Mwislamu huyo kutoka Japan anabainisha hivi moja ya sababu zilizompelekea kuikubali dini tukufu ya Kiislamu: ‘Katika zama ambazo nilikuwa bado sijauchagua Uislamu, kulikuwa na mjadala mkubwa kuhusu wasichana wanaovaa Hijabu katika shule za Ufaransa na mjadala huo ungalipo. Wengi waliamini kuwa shule za kiserikali Ufaransa hazipaswi kujihusisha na itikadi za kidini za wanafunzi. Mimi pia wakati huo nikiwa kama mtu asiyekuwa Mwislamu nilitafakakari na kujiuliza ni kwa nini wakuu wa shule wanachukua msimamo mkali kuhusu suala dogo kama vile mtandio wa wanafunzi.
Wasiokuwa Waislamu wamekuwa na dhana potofu kuwa wanawake Waislamu wanalazimishwa kutii sheria za Kiislamu na ndio sababu wanavaa Hijabu. Kwa msingi huo wasiokuwa Waislamu wamekuwa wakiitazama Hijabu ya wanawake Waislamu kama nembo ya dhulma na kudai kuwa uhuru wa mwanamke unapatikana tu kwa kutovaa Hijabu. Hii ni katika hali ambayo wanawake wengi wasiokuwa Waislamu duniani, baada ya kusilimu, hutazama uvaaji Hijabu kama sheria ya kimantiki kidini. Mimi pia ni mfano wa wanawake hawa. Hijabu yangu si sehemu ya utambulisho wangu wa kijadi au kirangi wala haina maana ya kisiasa au kijamii; Hijabu yangu ni utambulisho wangu wa kidini. Nilipoamua kuikumbatia dini ya Kiislamu, kamwe sikudhani kuwa siku moja ningeweza kusimamisha sala tano kwa siku au ningeweza kulinda Hijabu yangu. Raghba na hamu yangu ya kuwa Muislamu ilikuwa na nguvu kubwa kiasi kwamba sikuwa na wasiwasi kuhusu mabadiliko ambayo yalikuwa yanakuja.’
Bi. Nakata Khaula anasema hivi kuhusu nama alivyosilimu na kuvaa Hijabu: ‘Baada ya kusikiliza hotuba katika Msikiti wa Paris, nilifahamu faida za kuzingatia Hijabu kiasi kwamba hata baada ya kuondoka msikitini, niliendelea kuvaa mtandio ambao nilikuwa nimeuvaa kwa ajli ya kuuheshimu msikiti. Hotuba hiyo ilinighirikisha katika aina fulani ya ridhaa ya moyoni. Hii ilikuwa ni hali ya kipekee ambayo nilikuwa sijawahi kuihisi. Kwa hakika hisia hiyo ilinifanya nisitake kuondoka msikitini bila mtandio. Mavazi hayo yangu hayakuzingatiwa na watu wakati huo kutokana na kuwa hali ya hewa ilikuwa ya baridi kali. Pamoja na hayo nilikuwa na hisia nzito iliyoniambia kuwa nilikuwa tafauti na wengine, nilipata hisia ya utakasifu na usalama.’
Ingawa kabla ya kusilimu Bi. Nakata Khaula aliitazama hijabu kama kizingiti, lakini leo yeye ni mwanamke ambaye anazingatia kikamilifu Hijabu ya Kiislamu. Anayatazama mavazi yake kuwa yenye thamani ya kimaanawi na yanayoashiria imani yake ya kidini. Kuhusiana na hili anasema: “Kutokana na kuzingatia Hijabu ninapata furaha na ridhaa. Suala hili ni ishara ya kutii amri ya Mwenyezi Mungu na imani yangu. Hakuna tena haja ya kuitangaza itikadi yangu kwa sauti kubwa, Hijabu yangu inawabainishia wote imani yangu. Hijabu inawakumbusha watu kuwa Mwenyezi Mungu yupo na daima inanikumbusha kuwa mwenendo wangu unapaswa kuwa ule wa mwanamke Mwislamu. Ni sawa na maafisa wa polisi ambao wakiwa wamevalia sare zao za kazi, huwa waangalifu zaidi kwa hivyo mimi pia ninapovaa Hijab ninapata hisia zaidi ya kuwa Mwislamu.’

Kwa nini wanawake Ulaya, Marekani n.k wanasilimu?

Bi. Nakata Khaula anasema maisha yake akiwa Muislamu ni bora zaidi ya huko nyuma na anaamini kuwa pambo la mwanamke ni Hijabu. Bi.Khaula anasema maisha yake yamejaa heshima, utulivu na kujiamini kutokana na vazi la Kiislamu la Hijabu. Anabainisha umaridadi wa Hijabu ya Kiislamu ifuatavyo:
‘Kutazamwa Hijabu juu juu kutoka nje ni jambo ambalo huzuia kutambulika uhakika wa vazi hili. Mtu ambaye bila ufahamu anautazama Uislamu kutoka nje, yamkini anaweza kudhani kuwa Hijabu ni kizingiti katika maisha ya mwanamke Mwislamu. Lakini ukiitizama Hijabu ukiwa katika Uislamu unachopata si kingine ila ni utulivu, uhuru, ridhaa – ridhaa ambayo huko nyuma nilikuwa sijawahi kuipata. Wafuasi wa dini tukufu ya Kiislamu wameichagua dini hii badala ya uhuru potofu wa usekula. Sasa tunapaswa kuuliza, iwapo Uislamu ni dini inayomdhulumu mwanamke, ni kwa nini wanasilimu wanawake wengi vijana walio na masomo ya juu barani Ulaya, Marekani, Japan, Australia n.k.? Kwa hakika mwanamke mwenye Hijabu ana umaridadi wa malaika. Lakini taasubi iliyowapofusha baadhi ndio inayowapelekea kukosa kuona umaridadi huu.’
Katika kubainisha ukweli kuhusu vazi la Hijabu, Bi. Nakata Khaula ameandika kitabu kuhusu Hijabu kwa lugha ya Kiingereza chini ya anwani ya ‘A View Through Hijab.’

Hijabu ni pambo la mwanamke

Hijabu ya Kiislamu ambayo Bi. Nakata Khaula ameitaja kuwa ni pambo la mwanamke inatokana na mafundisho asili ya Kiislamu. Ili kuhifadhi usalama wa kiroho katika jamii na kuibua uhusiano salama baina ya mwanamke na manaume katika jamii na mazingira ya kazi, Uislamu unamtaka mwanaume na mwanamke wawe na mavazi kamili wakiwa katika harakati zao za kijamii ili jamii ambayo ni salama iweze kupiga hatua za ustawi na maendeleo.
Hijabu ya Kiislamu mbali na kuwa inainua shani ya mwanamke kutoka kiwango cha kutumiwa kama chombo, vile vile inampa moyo wa kujiamini na utambulisho mpya na hivyo kulinda hadhi yake ya kibinaadamu. Ni kwa sababu hii ndio wanawake wengi wenye masomo ya juu katika nchi za Magharibi wakaamua kusilimu. Hawa wanawake Wamagharibi wanaosilimu tayari huwa wameshapata kuona natija ya wanawake kutovaa hijabu na kuwa na uhuru usio na mipaka katika nchi zao. Wanaamini kuwa kile ambacho huwa wanapewa kwa jina la uhuru kwa hakika si uhuru. Mfumo wa familia katika nchi za Magharibi umeporomoka huku wanawake wakitumiwa na mabepari kama chombo cha kibiashara.
Katika mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu nafasi ya kibinadamu ya mwanamke na mama inaheshimiwa sana. Aidha katika Uislamu suala la familia na kujistiri limepewa umuhimu mkubwa. Kwa kifupi ni kuwa mwito wa Uislamu ni mwito wa kujibu mahitajio yote ya mwanaadamu. Mwito huu humpa mwanaadamu uhai halisi kama ambavyo Mwenyezi Mungu SWT anvyosema katika aya ya 24 ya Surat Al Anfaal: ‘ Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapo kuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu huingia kati ya mtu na moyo wake, na kwamba hakika kwake Yeye tu mtakusanywa.’

http://kiswahili.irib.ir