Kiislamu vyanzo

  1. home

  2. article

  3. Uislamu, Chaguo Langu 6 + Sauti

Uislamu, Chaguo Langu 6 + Sauti

Rate this post

Sikiliza

Heather Olmstead alizaliwa katika jimbo la Wisconsin la Marekani na sasa ameuchagua Uislamu kama njia bora zaidi na muongozo wa maisha yake.
Heather Olmstead anafafanua hivi kuhusu safari yake ya kuelekea katika Uislamu:
‘Mimi ni mwanamke Muislamu aliyesilimu. Tarehe 15 Agosti mwaka 2002 nilitamka shahada mbili. Jambo hili kwa hakika lilinifurahisha sana kwani maisha yangu yamekuwa bora kwa kufuata Uislamu. Katika umri wangu nimekuwa nikitafuta njia ya kumfikia Mwenyezi Mungu. Nilizaliwa katika familia ya Kikristo na daima nimekuwa nikitafuta haki na uongofu. Nilichunguza dini nyingi na sasa nimefikia ukweli huu wa Uislamu. Katika eneo ninaloishi wote ni Wakristo, lakini wote hawatekelezi Ukristo kivitendo. Katika shule ya sekondari niliyosoma kulikuwa na Wakristo wachache ambao walitekeleza vyema mafundisho ya dini yao. Nilikuwa nikifanya mijadala na hao Wakristo kuhusu Bibilia na kila mwisho wa wiki tulikuwa tukienda makanisani. Ili kupata ukweli, nilifanya utafiti kuhusu makundi mbali mbali ya Kikristo. Nilifanya utafiti kuhusu utawa na hata kuhudhuria ibada zao. Baada ya hapo nilijifunza kuhusu Ukatoliki na nikaamua kuwa mtawa. Nilianza kushiriki katika masomo ya kidini ya Ukatoliki lakini nilikuwa sijateuliwa rasmi kuwa mtawa. Katika chuo kikuu nilichagua taaluma ya thiolojia ambapo niliegemea katika utafiti linganishi wa dini.

Matukio ya Septemba 11 yalinielekeza katika Uislamu
Utafiti kuhusu dini uligeuka na kuwa sehemu ya maisha yangu. Kadiri nilivyosoma niligundua upungufu zaidi katika Ukristo. Niliamua kuchukua hatua kuelekea katika ulimwengu ulio nje ya Ukristo. Nilijifunza na kufanya utafiti kuhusu itikadi za dini kama vile Uhindu, Ubudha, Ubahai na Uyahudi. Hata baadhi ya wakati nilitekeleza ibada za dini hizo. Lakini kufika katika Uislamu ulikuwa muujiza uliojitokeza kupitia matukio ya Septemba 11 mwaka 2011.’
Bi. Heather Olmstead anaendelea kusema: ‘Kutokana na uongo ulioenezwa na vyombo vya Magharibi kufuatia matukio ya Septemba 11 na propaganda potofu dhidi ya Waislamu, nilitaka kujua zaidi kuhusu Uislamu. Sawa na maelfu ya wengine wasiokuwa Waislamu nilianza kufanya utafiti kuhusu mafundisho ya Uislamu.’
Bi. Olmstead anasema hivi kuhusu taathira za propaganda potofu za Magharibi dhidi ya Uislamu: ‘Baada ya kusikiliza propaganda hizo nilidhani Uislamu ni dini ya ubabe, yenye kumdhulumu mwanamke na itumiayo mabavu. Hadi sasa wengi bado wana dhana hii potofu. Katika kipindi chote cha utafiti wangu kuhusu dini mbali mbali, niliutazama Uislamu kama somo tu la kidini. Pamoja na kuwa vyombo vya habari viliendelea kueneza taswira isiyo sahihi kuhusu Waislamu, niliamua kufanya utafiti ili kujua ukweli. Sikuwa na maelezo kamili kuhusu Uislamu. Nilihisi kuwa ninapaswa kufuata ukweli. Baada ya muda usio mfrefu niligundua tovuti moja ya Kiislamu na hapo nikatuma barua pepe nikitaka nitumiwe vitabu kuhusu Uislamu. Baada ya kusoma vitabu hivyo, nilishangaa sana. Hii si ile dini niliyokuwa nikidhani.
Muujiza wa Qur’ani katika maisha yangu
Mmoja wa wasimamizi wa tovuti hiyo alinifanyia wema na kunitumia tarjumi ya Qur’ani Tukufu kwa lugha ya Kiingereza. Baada ya kuisoma, nilihisi imetulia katika moyo wangu na kwamba nimeingia katika njia ya kumridhisha Mwenyezi Mungu. Pamoja na kuwa nilikuwa nimetenga masaa kadhaa ya kufanya utafiti wa intaneti kuhusu Uislamu, niliamua kuwa kabla ya kutoa shahada mbili, nitahitimisha Qur’ani. Katika kipindi chote hicho cha kuisoma Qur’ani sikukumbana na chochote ambacho kingeniweka mbali na imani yangu. Kinyume chake, niliona mengi katika Uislamu ambayo nilikuwa ninayaamini na nikahisi kana kwamba Mwenyezi Mugu amekuwa akiniongoza kuekelea katika Uislamu katika kipindi chote cha maisha yangu.’
Muujiza wa Qur’ani kwa mtazamo wa maudhui, ufasaha, balagha na mvuto wake wa Kiislamu ni mambo ambayo yanaendelea kuvutia nyoyo za watafutao ukweli kuelekea katika njia ya Mwenyezi Mungu. Mvuto huu ni mkubwa kiasi kwamba njama za wapinzani na maadui si tu kuwa hazijaudhoofisha Uislamu bali zimepelekea ukweli wake kudhihirika wazi zaidi.
Baada ya matukio ya Septemba 11 mwaka 2001, kwa kunasibisha suala hili na Waislamu, rais wa wakati huo wa Marekani George W Bush alitaja vita vya kile kinachodaiwa kuwa ni ugaidi kuwa ni vita vya msalaba. Baada ya tamko hilo viongozi na shakhsia wenye misimamo mikali wa Marekani na Ulaya walianzisha harakati za kuwadhalilisha na kuwavunjia heshima Waislamu.
Hata William Cohen Waziri wa Zamani wa Ulinzi Marekani aliwahi kusema kuwa kukabiliana na Uislamu ni vita vya nne vya dunia.
Ni katika hali hiyo ndio Marekani ilizivamia kijeshi na kuzikalia kwa mabavu nchi za Kiislamu za Iraq na Afghanistan na sambamba na hayo kuzidisha vita vya kipropaganda dhidi ya Waislamu kote duniani. Lakini nukta ya kuzingatiwa hapa ni hii kuwa, njama hizi dhidi ya Waislamu ambazo zingali zinaendelea, zimekuwa na natija kinyume na ilivyotarajiwa kwani idadi kubwa ya watu duniani sasa wanavutiwa zaidi na Uislamu.
Mtazamo wa Wamaharibi kuhusu mafundisho ya juu na yenye kumjenga mwanaadamu ya Kiislamu ndio nukta muhimu zaidi ya propaganda za kuupiga vita Uislamu. Hii ni kwa sababu, kwa kuujua Uislamu kila mtu hufahamu namna Uislamu unavyounga mkono amani, uadilifu, mapenzi na wakati huo huo kupinga vikali kuua watu wasio kuwa na hatia. Katika Qur’ani Tukufu tunasoma kuwa mtu anayemuua mwenzake asiye na hatia ni kana kwamba amewaua watu wote. Aidha katika aya na riwaya nyingi suala la kufanya mazungumzo na kustahimiliana na wengine limesisitizwa sana.
Nilisema ‘Labaik’ kwa wito wa Allah SWT
Bi. Heather Olmstead, baada ya juhudi na utafiti kuhusu kujikuribisha mbele ya Mwenyezi Mungu, aliukubali Uislamu na kusema Labaik kwa wito wa Allah SWT. Anafafanua hivi kuhusu utamu wa Labaik yake: ‘Hatimaye 15 Agosti mwaka 2002 nilitamka ‘La ilaha ila Allah, Mohammad Rasulullah’ na nikawa Mwislamu. Nilikuwa na hisia ya hali ya juu sana.’
Uislamu ni dini yenye kuleta mabadiliko kamili katika maisha ya kila anayesilimu na kufuata mafundisho yake. Uislamu uko katika kila sekta ya maisha ya mwanaadamu. Dini hii tukufu daima inawaita watu kuekelea katika rehema ya Mwenyezi Mungu na hairuhusu kutokuwa na matumaini.
Katika aya ya 53 ya Sura Azzumar tunasoma hivi: Sema: Enyi waja wangu walio jidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.

http://kiswahili.irib.ir