Kiislamu vyanzo

  1. home

  2. article

  3. Umuhimu wa Kazi Katika Uislamu (4)

Umuhimu wa Kazi Katika Uislamu (4)

Rate this post

Bismillahir Rahmanir Rahim

Mifumo ya kiuchumi duniani ukiwemo mfumo wa kiuchumi wa Uislamu, una misingi ya kifalsafa na mtazamo wake maalumu kuhusiana na dunia. Kama tulivyosema katika kipindi chetu kilichopita kilichokujieni kabla ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni kuwa, katika mtazamo wa Uislamu, itikadi na imani za mtu zina nafasi ya kimsingi katika maisha yake. Kwa muktadha huo, miamala ya kiuchumi yaMuislamu ina uhusiano na mfungamano wa karibu mno na masuala yake ya kiitikadi na kiakhlaqi (kimaadili). Kwa maneno mengine ni kuwa, katika Uislamu masuala yote ya maisha ya mwanaadamu yakiwemo masuala ya kiuchumi yameainishwa na kuundika katika fremu ya mafundisho ya dini. Katika mtazamo wa Uislamu, mwanaadamu ni kiupmbe mwenye engo mbili za kimaada na kimaanawi. Mwenyezi Mungu alimuumba mwanaadamu na kumfanya kuwa kiumbe bora miongoni mwa viumbe wake na kamtukuza mwanaadamu huyu ili kiumbe huyu atumie kipaji chake alichonacho kwa ajili ya kufikia katika ukamilifu wa kiroho na kimaanawi. Si hayo tu, bali Mwenyezi Mungu akamuandalia mazingira mwanaadamu huyu pamoja na suhula na nyenzo za lazima ili aweze kufikia lengo hilo na wakati huo huo akidhi mahitaji yake ya kimaada na kimaanawi. Ili mwanaadamu aweze kukidhi mahitaji yake ya maisha hana budi kufanya kazi. Mintarafu hiyo ndio maana kufanya kazi katika Uislamu ni jambo lenye thamani na ambalo limetiliwa mkazo na kukokotezwa mno. Kufanya kazi na kujituma kwa ajili ya kutafuta riziki ya halali ni moja ya nguzo za saada ya mwanaadamu katika dunia hii na kesho akhera. Tukiirejea Qur’ani Tukufu tunapata kuwa, kuna aya zaidi ya 80 ambazo zinabainisha kwamba, sharti la saada na ufanisi wa mwanaadamu ipo katika mambo mawili imani na kufanya amali njema. Kufanya kazi na kujihimu kwa ajili ya kudhamini mahitaji ya maisha kwa kutumia wakati na kustahamili mashaka na taabu ni miongoni mwa amali njema na zinazomridhisha Mwenyezi Mungu SW. Hata hivyo katika Uislamu, kila amali na kazi ambayo inafanyika kwa ajili ya kufikia malengo sahihi, inahesabiwa kuwa kazi yenye thamani kubwa. Mhandisi ambaye anachora michoro katika karatasi kwa ajili ya kuandaa ramani ya jengo, michoro ambayo inamchukulia muda wake mwingi na fikra zake, mchoraji ambaye anachora mandhari nzuri katika ubao, mhadhiri ambaye anashughulika na kufundisha katika Chuo Kikuu au mtunza bustani na mkulima ambaye anajishughulisha na kazi ya kulima wote hao kutokana na kufanya kwao hima na idili kwa namna moja au nyingine wanakuwa na ushiriki amilifu katika ustawi na maendeleo ya jamii.
Kiujumla ni kuwa, kazi ya kiuchumi kwa mtazamo wa Uislamu inaweza kuarifishwa na kutambulishwa namna hii: “Ni kila harakati na kazi inayofanyika kwa ajili ya uzalishaji bidhaa za mahitaji au kupeleka juu uwezo wa jamii na kuboresha hali jumla ya jamii katika fremu ya sheria na thamani na kidini inahesabiwa kuwa kazi ya kiuchumi.”
Kimsingi kazi ni nguzo muhimu na ya kimsingi kwa ajili ya mtu kujipatia kipato cha kuendeshea maisha yake. Katika aya nyingi Qur’ani Tukufu sambamba na kukumbusha vyanzo na suhula zilizoko katika ulimwengu inamshajiisha mwanaadamu kuboresha ardhi kwa ajili ya kukidhi mahitaji yake ya kimaisha na inabainisha umuhimu wa suala hilo katika nyanja mbalimbali.
Katika Qur’ani Tukufu kuna aya nyingi ambazo zinamkumbusha mwanaadamu neema alizopatiwa na Mwenyezi. Kwa mfano tunasoma katika aya ya 20 ya Surat Luqman kwamba:
“Kwani hamwoni ya kwamba Mwenyezi Mungu amevifanya vikutumikieni viliomo mbinguni na kwenye ardhi, na akakujalizieni neema zake, za dhaahiri na za siri…?”
Katika aya nyingine Mwenyezi Mungu anaeleza kuwa, mbingu, ardhi, milima, bahari, mito na wanyama vimeumba na viko kwa ajili ya mwanaadamu na kiumbe huyu anapasa kustafidi na vitu hivi kwa ajili ya kuboresha maisha yake.
Wassalamu Alaykum Warahmatulahi Wabarakatuh

http://kiswahili.irib.ir