Kiislamu vyanzo

  1. home

  2. book

  3. JE, MUNGU ATAONEKANA? [Mjadala wa Kiitikadi, na Kifalsafa kwa mujibu wa Qur’ani na Sunnah]

JE, MUNGU ATAONEKANA? [Mjadala wa Kiitikadi, na Kifalsafa kwa mujibu wa Qur’ani na Sunnah]

  • MUHAMMAD O. ALY ZENJIBARY
  • ZANZIBAR TANZANIA
download

    Download

Rate this post
description book specs comment

Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu, Muumba wa dunia hii,
Rehma na amani zimshukie Mtukufu Mtume (s.a.w.) pamoja na ahli
zake wote.
Qur’ani tukufu inawataka wanaadamu kutafakari na kuzingatia hasa
katika vile vilivyoumbwa na Mungu ili waweze kuzielewa siri za
maumbile.
Mwanadamu anatakiwa aifikirie hali yake, matendo yake na nafsi yake.
Kuzingatia matukio ya kihistoria kunapelekea kuweza kuelewa asili ya
mambo yalivyo.
Hivyo, Uislamu unaiona tauhidi ambayo, ndiyo kielelezo hasa cha
upweke wa Mungu, kama jambo la msingi ambalo ni wajibu
kulitafakari na kulizingatia.
Imepokewa kutoka kwa Abu Abdillah (a.s.), kuwa siku moja Imam
Ali (a.s.) alipokuwa anahutubu juu ya Mimbar ya msikiti wa mji wa
Al-Kufa, huko Iraq, mtu mmoja aliyeitwa Daalabu alisimama na
kumuuliza haya:
“Ewe Amiirul-muuminiin, umewahi kumwona Mola wako?”
Imam akasema: “Ole wako ewe Daalab, mimi siwezi kumuabudu
Mungu nisiyemuona”. Daalab akasema: “Ewe Imam, umemuonaje?”
Imam akajibu kwa kumwambia:
“Ewe Daalab, elewa kuwa macho hayawezi kumuona kwa kumtazama
bali nyoyo ndizo zinazomuona kutokana na ukweli wa imani…”
1
ُ“Macho hayamfikii kumuona bali Yeye anayafikia macho, naye ni
Mwenye kujua (ya ndani) Mwenye khabari.”2
Upweke wa Mwenyezi Mungu ni nadharia isiyo shaka na ipo haja ya
1 Kutoka kitabu “A Shiite Anthology” cha Allamah Sayyid Muhammad Husayn Tabatabaiy,
uk. wa 38-39.
2 Suratul An’aam, aya ya 103
2
kueleza mipaka ya asili ya kumpwekesha Allah (tawhid) na ile mipaka
inayopelekea ushirikina (shirk), jambo hili linahitajia vielelezo na
mazingatio makubwa kwa vile ndio hasa mzizi mkuu wa dini yenyewe.
Qur’ani imewasisitiza watu kutafakari kwenye maumbile na maajabu
yake ili wapate kumuelewa Muumba hasa wa maumbile hayo. Mara
nyingine Qur’ani huashiria hayo kwa kusema:
ِ“Hakika katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi, na katika kupishana
kwa usiku na mchana, na katika vyombo vipitavyo baharini kubeba
yale yenye faida kwa watu, na katika maji aliyoyateremsha Mwenyezi
Mungu kutoka mawinguni ambayo kwayo ameihuisha ardhi baada
ya kuchakaa, kisha akaeneza humo aina zote za wanyama, na katika
mabadiliko ya pepo na mawingu yaliyoamriwa kupita baina ya mbingu
na ardhi; bila shaka katika haya zimo ishara kwa watu wenye
kuzingatia.”
3
Mwislamu anatakiwa azingatie haya yote ili aelewe uwezo, sifa, na
hatimaye dhati
4
ya Mola wake. Inasikitisha kuona kuwa Waislamu sasa
wameiacha falsafa hii ya kutafakari kwa kutumia vipaji na akili zao.5
3 Suratul Baqarah, aya ya 106
4 Dhati ya Allah haieleweki. Kwa hivyo, jua ndugu msomaji kwamba makusudio yangu juu ya
kuijua dhati ya Allah, ni vile kutokuijua kwani, kama ilivyosemwa, kutokumdiriki Allah ndio
kumdiriki kwenyewe.
5 Sikusudii kusema kwamba tuitangulize akili kuliko Sharia, bali nakusudia kusema kwamba
tutumie akili katika kuisoma Sharia, kwani Sharia haigongani na akili. Naam! Yako mambo
ambayo akili ya binaadamu haina uwezo wa kuyafahamu. Mambo haya ni baadhi ya mambo
ya Sharia: si mambo ya kiakili. Mfano wa hayo ni kama vile ni kwa sababu gani tusali rakaa
mbili alfajiri na nne adhuhuri; kwa nini tuzunguke al-Ka’aba n.k. Lakini, tena, elewa kwamba
kuna tofauti baina ya mambo ambayo yanagongana na akili na mambo ambayo akili haina
uwezo wa kuyafahamu. Mambo hayo tulioyataja hapo si kwamba yanagongana na akili bali
ni mambo ambayo akili ya kiumbe haiwezi kuyafahamu. Ama mambo yanayohusiana na sifa
za Allah ni mambo yanayofahamika kiakili. Huoni kwamba akili timamu haihitaji andiko ili
kujua kuwa Allah ndiye Muumba, Muweza, Mwenye elimu n.k.
Matokeo ya jambo hili ni kwamba kumepatikana watu wanaokataa
kabisa kutumia akili zao katika Uislamu. Kwa ajili ya hayo
kukapatikana Waislamu wanaoitwa “ahlu-dhwahiri”, ambao ni wale
waliozichukua hadithi, aya na ibara nyingine kama zilivyo katika maana
yake ya juu juu au ya dhahiri. Kuna wengine huitwa “ahlul-hadith”.
Wengine wakajiita “as-salafiyyah”. Bali hawa walikataa hata kuzifanyia
taawili baadi ya aya za Qur’ani ili kupata maana sahihi inayokubaliana
na fikra ama akili zilizoumbwa na Mungu.
Hayo ndio mambo yaliyotukumba.
Qur’ani inasema kinaga ubaga kuwa:
َ“Hakika sisi tumeiteremsha Qur’an kwa lugha ya Kiarabu ili mpate
kuifahamu”.
Iwapo Qur’ani imeshuka kwa lugha ya kiarabu, ni lazima fani na fasihi
ya lugha hii imetumika katika Qur’ani; na iwapo haya ni kweli, kwa
nini tukatae kuwa katika Qurani mna majazi, istiara, na fani nyingine
za balagha? Kwa kuwa Kiarabu hakiachani na fani hizi, kwa nini sisi
tuzikatae fani hizi tunapofasiri Qur’ani?
Suala la kuonekana ama kutoonekana kwa Mwenyezi Mungu huko
Akhera limezuka kutokana na na matatizo mawili:
Moja ni kutokuzichuja riwaya zilizosimuliwa juu ya maudhui hii, kwa
kuzitazama sanadzake na matinizake ambapo Qur’ani ilitakiwa iwe
ndio kipimo cha mwanzo cha kuzipima riwaya hizo.
Pili ni tatizo hili tulilolitaja hapa la kutokwenda kwa mujibu wa fani za
lugha ya Kiarabu.
Kuzifasiri aya za Qur’ani bila ya kujali taratibu za asili ya lugha ya
Kiarabu ni kupotosha Qur’ani yenyewe.
6 Surat Yusuf, aya ya 2.
Katika kitabu hiki suala la kuonekana kwa Mwenyezi Mungu na
macho ya wanaadamu huko Akhera limepingwa kutokana na
kukosekana kwa ushahidi wa Qur’ani na Sunna za Mtukufu Mtume
(s.a.w.w.). Pia aya zilizotumiwa kama ni ushahidi wa kuthibitisha
kuonekana kwa dhati ya Allah zimeelezwa na kufafanuliwa muradi
wake na makusudio yake. Kwa kifupi aya zinazodaiwa na baadhi ya
Waislamu kuwa zinathibitisha kuonekana kwa Mungu kwa macho
huko Akhera unapozipeleka kwenye fani za lugha yenyewe, maana haya
haitakubalika kwa vile zinapingana na aya nyingine kama utakavyoona
hayo wewe mwenyewe.
Kwa kuwa sisi Waislamu makimbilio yetu ni Qur’ani tukufu mjadala
huu tumeuacha na kuukabidhi kwa Qur’ani ili tupate uamuzi sahihi.
Ni matumaini yangu kuwa kitabu hiki kitachukuliwa kama ni
chimbuko la kubadilishana mawazo tu wala si ushabiki na tusi kwa
yeyote.
Nitakuwa mwizi wa fadhila kama nitaacha kumshukuru ndugu yangu
Sheikh Juma Mazrui wa Oman aliyetoa mawazo yake mengi kwangu
katika kukamilisha Kitabu hiki kwa lengo la kuufikisha ujumbe huu
wa Qur’ani Tukufu. Kwa hakika Sheikh Juma Mazrui amechukua
bidii kubwa katika kuniongezea dondoo ambazo katika mazingira
niliyokuwa nikiishi ilikuwa ni tabu sana kupata dondoo hizo, kuna
uchache wa vitabu hapa nilipo, na wakati wa kutafiti kwangu ulikuwa
mdogo kutokana na sababu zisizoweza kuzuilika.
Hakika namuomba Allah azidi kumpa Sheikh Juma Mazrui ufanisi
na tawfiiq Duniani na Akhera ili aendelee kushirikina na waisilamu
wenzake bila ya kujali rangi zao, kabila zao na madhehebu
wanayofuata.Hakika sifa hii ya Sheikh Juma inapaswa kuigwa na
kupigiwa mfano. Kama kulikuwa na malumbano ya kimadhehebu
baina yangu na Sheikh Juma Mazrui miaka iliyopita ilikuwa amma
ni kutokana na shetani au kutokana na nafsi zetu ambazo zilikuwa na
hadi leo hii hazijakamilika, lakini nachukua nafasi hii kumlaani
shetani na kumweka mbele Allah Subhanahu wataala kwa kila jambo,
na namuomba Allah akijaalie Kitabu hiki kiwe ni sababu ya
kuwaunganisha waisilamu wote Duniani, amin.
Kwa hakika Sunni, Salafi, Shia na Ibadhi wote ni Waisilamu
wanaohitajiana na inshaallah Kitabu hiki kitakuwa ndio ni moja ya
funguo za fikra ya mlingano na kukurubiana na kuondoa tofauti kati
ya waisilamu inshaallah. Ukamilifu wote ni wa Allah na kama kukiwa
na kasoro yoyote kwenye kitabu hiki, kasoro hiyo inatoka kwangu
natanguliza kuomba msamaha kwa kasoro hizo kwa Allah na kwa
waisilamu wote.

  • MUHAMMAD O. ALY ZENJIBARY
  • ZANZIBAR TANZANIA