Kiislamu vyanzo

 1. home

 2. book

 3. SHIA NA QURANI MAJIBU NA MAELEZO

SHIA NA QURANI MAJIBU NA MAELEZO

 • Abdilahi Nassir
 • Bilal Muslim Mission of Tanzania
 • Dar es Salaam - Tanzania
download

  Download

Rate this post
description book specs comment

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehema na amani zimshukie
bwana wetu na mwombezi wetu, Muhammad b. Abdillahi, na ali zake wema
waliotakaswa wakatakasika, na wote wanaofuata nyayo zao.
Hitilafu baina ya Shia na Waislamu wengine wasio Shia haikuanza juzi na
jana. Ilianza karne nyingi zilizopita; mara tu baada ya Mtume Muhammad
s.a.w.w. kufariki dunia. Hata hivyo, katika kipindi cha Makhalifa wawili
wa kwanza, hitilafu hiyo haikuzusha zogo na fitina kubwa kama lile
lililozuka katika kipindi cha Makhalifa wa tatu na wa nne. Na hilo ni kwa
sababu ambazo, kwa kuwa ziko nje ya maudhui ya kitabu hiki, sikusudii
kuzizungumzia humu. Itoshe tu, kwa hivi sasa, kujua kwamba ni baada ya
Khalifa wa tatu (Khalifa Uthman) kuuliwa, na mtu aliyekiitwa Muawiya
kuongoza upinzani dhidi ya Khalifa wa nne (Imam Ali), ndipo hitilafu
hiyo ilipopaliliwa moto. Na kutokana na upinzani huo ndipo Imam Ali a.s.
alipolaaniwa, kwa amri ya Muawiya, katika hotuba zote za Ijumaa, kwa muda
usiopungua miaka themanini. Ndipo wote wale waliokimtambua Imam
Ali a.s. kuwa ni imamu wa haki (yaani Shia) walipokuwa wakisakwa kama
nyoka na kuuawa! Ndipo Imam Hassan a.s., mjukuu wa Mtume s.a.w.w.,
alipouliwa kwa kutiliwa sumu chakulani mwake! Ndipo Imam Hussein a.s.,
mjukuu mwingine wa Mtume s.a.w.w., alipouliwa kinyama huko Karbala
(Iraq) kwa kukatwa kichwa chake, kikatungikwa kwenye mkuki na
kuchezewa ngoma, na kuliacha pingiti la mwili wake lishetwe-shetwe
na farasi! Ndipo hofu ilipofikia kiwango cha watu, chini ya Ufalme wa
Muawiya, kuogopa kuwapa watoto waliowazaa jina la Ali! Ndipo hata
mashekhe, kwa kuchelea kuadhibiwa na kuuawa, walipokiogopa kulitaja
jina la Imam Ali a.s. katika riwaya za Hadith za Mtume s.a.w.w.; badala yake
ikawa husema: ‘Amesema Sheikh’!
Hapo ndipo chuki baina ya Shia na wasio Shia ilipozidi na kuendelea kwa
miaka mingi – mara inapanda, mara inashuka – hadi hii karne tuliyonayo.
Katika karne hii, kiasi cha miaka thelathini hivi iliyopita, baadhi ya
wanazuoni wa Kishia na wasio Shia huko Mashariki ya Kati wakaona la!
Hali hii haifai kuachwa ikaendelea. Kwa hivyo wakakutana na kujadiliana
jinsi ya kuleta mkuruba na uelewano baina ya madhehebu mbali mbali ya
Kiislamu – hasa baina ya Shia na Sunni. Matokeo yake yakawa ni kuundwa
chama kilichoitwa Darut Taqrib Baynal Madhahibil Islamiyyana kuweka
jukwaa la pamoja la kuwawezesha wanazuoni hao wa madhehebu mbali
mbali kueleza imani na misimamo ya madhehebu yao juu ya mada mbali
mbali za kidini.
Hatua hii ilisaidia sana kuleta uelewano kiasi cha kwamba, Sheikh
Mahmud Shaltut (aliyekuwa Mufti wa Al-Azhar wakati huo) alitoa ile
fatwa yake mashuhuri ya kusema kwamba madhehebu ya Ja’fari (yaani
Shia Ithna-ashari) ni madhehebu ya Kiislamu yanayojuzu kufuatwa katika
kufanyia ibada kama madhehebu mengineo ya Sunni. Na, kwa mara ya
kwanza akaruhusu madhehebu hayo yasomeshwe katika Chuo Kikuu hicho
cha Al-Azhar huko Misri.
Hata hivyo, baadhi ya masheke wa wakati huo hawakupendezwa na hatua
hiyo. Miongoni mwao ni mmoja aliyekiitwa Muhibbudin al-Khatib. Huyu
aliandika kitabu kwa lugha ya Kiarabu kiitwacho al-Khututul Aridhwa
kuonyesha kwamba ni muhali jaribio hilo la wanazuoni wenzake kufanikiwa –
hasa inapokuja kwenye uelewano baina ya Sunni na Shia – na akatoa sababu
zake. Sababu hizo ndizo tutakazozijadili katika mfululizo wa vitabu vyangu
hivi inshallah, kuanzia ile inayohusu Qur’ani Tukufu.
Japokuwa kitabu hicho kishajibiwa kwa hiyo hiyo lugha ya Kiarabu,
inaonekana kwamba wale wasiopendelea umoja baina ya Waislamu
hawana habari ya majibu hayo, au labda hawapendi kuwa nayo! Maana
kama si hivyo, wasingekuwa wakiendelea kukichapisha kitabu hicho mumo
kwa mumo, na kukifasiri kwa lugha nyinginezo, bila ya kusema chochote
juu ya majibu yaliyokwisha kutolewa.
Ilipofika 1983, miaka minne baada ya mapinduzi ya Kiislamu ya Iran,
kitabu hicho kilifasiriwa kwa Kiingereza na kusambazwa ulimwengu
mzima. Kwa nini? Kwa sababu ya waandamizi wa marehemu Sheikh M.
al-Khatib kuona jinsi juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zilivyofanikiwa
nje ya Ulimwengu wa Kiarabu, ambako lugha ya Kiingereza hueleweka zaidi,
katika kuleta uelewano na umoja baina ya Waislamu.
Huku kwetu Afrika Mashariki, tafsiri hiyo ya Kiingereza ilienezwa zaidi
kuliko ile nuskha ya Kiarabu – hasa miongoni mwa wanafunzi wa mashule
na vyuo vikuu. Hata hivyo, baada ya kuonekana kwamba athari ya nuskha
hiyo ya Kiingereza haikuwa kama ilivyotarajiwa, bali Waislamu wamezidi
kuvutiwa na maongozi ya Kiislamu ya Imam Khomeini na kutaka kujua
zaidi Ushia, jamaa hao wakaonelea bora itolewe tafsiri ya Kiswahili:
hwenda ikaleta athari itakikanayo! Hivyo hivi majuzi (Disemba 1988)
kukachapishwa tafsiri ya Kiswahili ya kitabu hicho kwa jina la Misingi
Mikubwa Iliyojengewa Dini ya Ushiaambapo kitabu hiki inshallah ndiyo
mwanzo wa majibu yake.
Katika kuandika majibu haya, napenda ieleweke kwamba sikuyaandika
kwa hiari; nimelazimika! Sikuyaandika kwa hiari kwa sababu ninaamini
kwamba kuna mambo muhimu zaidi, yenye manufaa na Waislamu
kwa jumla, ambayo sisi waandishi wa Kiislamu wa leo inatupasa
kuyashughulikia. Na nimelazimika kwa kuona hatari ya mfarakano baina
ya Waislamu inayoweza kutokea kwa vitabu kama hicho cha Sheikh M.
al-Khatib kuachwa bila ya kujibiwa – hasa hivi ambavyo idadi ya Shia
wananchi, humu mwetu Afrika Mashariki, inavyozidi kukua, na hasa hivi
ambavyo sababu zote alizozitoa shekhe wetu huyo katika kitabu chake
hicho hazina mashiko. Hivyo nimeyaandika majibu haya ili kuuzuia
mfarakano huo unaoweza kutokea; na kwa roho hiyo hiyo nakuomba, ewe
ndugu msomaji, uyasome.
Pengine, wakati mwingine, ushahidi utakaotolewa katika mfululizo wa
majibu haya utaonekana mkali. Hilo ni kweli! Lakini huo ni ukali usioweza
kuepukika! Ni kama daktari mpasuaji kulazimika kukikata kiungo kimoja
cha mwili ili kuuhifadhi mwili mzima. Mwili hapa ni umoja wa Waislamu,
na kiungo ni Sheikh M. al-Khatib na wale wenye mawazo kama yake.
Nataraji ndugu zangu mtayasoma majibu haya kwa ikhlasi na bila chuki,
pamoja na kuyalinganisha na vitabu nilivyovitolea ushahldi, ili mweze
kuufikia ukweli. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi.

 • Abdilahi Nassir
 • Bilal Muslim Mission of Tanzania
 • Dar es Salaam - Tanzania