Kiislamu vyanzo

Jumapili ya tatu ya mwezi wa Januari ndiyo siku ya Ulimwengu ya Madhehebu na ni  kwa munasaba huu ndipo tukapenda kuviangazia vipote vilivyomo katika madhehebu za kiislamu. Tofauti zilizopo kati ya madhehebu za kiislamu zinatokana ima na mambo ya kiakida na Imani au masuala ya kifikihi. Hivyo utapata kwamba kugawanyika kwa madhehebu ya kiislamu kunafuata misingi miwili mikuu:

Msingi wa kwanza: mgawanyiko  utokanao na tofauti za kiakida ambapo tofauti kuu zaidi hapa ni suala la mrithi wa mtume s.a.w.w. Katika suala hili tunayapata makundi mawili makuu ya kiislamu. La kwanza ni Ahlul Sunnati wal Jamaa’ah wanaoshikilia itikadi ya uadilifu wa maswahaba wote wa mtume s.a.w.w na wanao msimamo ya kuwa mtume hakumteua yeyote kumrithi ila aliwaachia waislamu jukumu hilo la kumchagua kiongozi wao baada ya kufariki kwake mtume s.a.w.w. Dalili yao  ni ( ijmaa’) kuafikiana kwa watu wa Madina na kwamba maswahaba wakubwa walikuwa wakiifanyia kazi rai hii.

Kundi la pili ni wafuasi wa Ahlil Bait ambao wanaamini kuwa yapo mapokezi hasa ya kuthibitisha kuwa ukhalifa baada yake mtume ni haki ya Ali mwana wa Abi Talib (karramallahu wajhahu) na wanawe. Dalili yao juu ya hili ni hadithi ya Ghadir na ile hadithi itajayo kwamba idadi ya makhalifa baada ya mtume ni 12. Ni kwa sababu ya hili ndipo wakaitwa ithashariyyah.

 

Waama madhehebu ya kiislamu kwa misingi ya tofauti za kifikihi yamejigawa vipote vitano ambapo kwa mujibu wa fatwa ya Sheikh Muhammad Shaltut, aliyekuwa shekhe wa Al Azhar, yeyote afuataye misingi ya lolote katika mapote haya matano yuko sawa na matendo yake ni sahihi. Madhehebu matano haya ni Malikiy, Hanafiy, Shaafi’iy, Hanbaliy na Ahlul Bayt ( Ja’fariy).

Madhehebu ya Maalikiy: Hunasibishwa na Abi Abdillahi Maalik bin Anas bin Abi Aamir Al Aswbahiy aliyezaliwa mjini Madina mnamo mwaka wa 93 Hijiria. Huyu alianza masomo udogoni chini ya uangalizi wa waalimu wake kama maulaa Abdullah bin Umar na wengineo. Hatimaye mnamo mwaka wa 179 hijiria aliaga dunia mjini Madina na kuzikwa Albaqii’.

Madhehebu ya Hanafiy: Hunasibishwa na Imam Abi Hanifah Annu’maaniy bin Thabit bin Al Taimiy Alkufiy aliyezaliwa mnamo mwaka wa 8 wa Hijiria. Alikuwa mwanazuoni mkubwa na alijulikana sana kwa matumizi yake ya Qiyas katika mambo ya kifikihi. Inasemekana kuwa Mansur Abbasiy alimpendekezea cheo cha ukadhi katika serikali yake ila Abu Hanifa akakataa. Kwa sabau hii basi Mansuru akamtia jela. Alifariki mnamo mwaka wa 150 Hijiria.

Madhehebu ya Shafi’iy: Hunasibishwa na Imam Abi Abdillah Muhammad bin Idris Qarashiy Shaafi’iy aliyeazaliwa mwaka wa 140 Hijiria katika mji wa Ghaza alipofikia umri wa mikaka miwili mama yake alimleta Makka na ndipo alipoishi hadi kifo chake katika mwaka wa 204 Hijiria akiwa na umri wa miaka 54.

Madhehebu ya Hanbali: hunasibishwa na Ahmad bin Hanbal bin Hilaal Aldhihliy Alshaibaaniy, ambaye alizaliwa Baghdaad katika mwaka wa 164 Hijiria. Aliwahi kusafiri kwenda Hijaz, Damascus na Yemen ambako alijishughulisha na masomo. Alikuwa mmoja wa wanafunzi wa Shaafi huko Baghdad.

 

Madhehebu ya Ahlulbayt / Jafariya / Imamiya: Hunasibishwa na Abu Abdillahi Jafar mwana wa Muhammad al Bakir mwana wa Ali Zainulabidin mwana wa Hussein mwana wa Ali bin Abi Talib kupitia kwa mbora wa wanawake wa duniani na akhera Fatima Zahra  binti yake mtume Muhammad (s.a.w.w.). Alizaliwa katika mwaka wa 83 Hijiria na ndiye imamu wa sita wa mashia ithnashariyyah naye ana watoto kumi, saba wa kiume na watatu wa kike. Alisifika kuwa mwingi wa elimu na uchamungu na pamoja na hayo alikuwa mwandishi wa vitabu vingi. Zaidi ya wanafunzi 4000 walihudhuria darasa zake za Hadith, Fikihi, Tafsiri na nyinginezo. Aliishi katika mji wa Madina na katika mji wa Baghdad kwa muda. Alifariki katika mwaka wa 10 wa utawala wa Mansur sawa na mwaka wa 148 Hijiria na kuzikwa katika makaburi ya Baqi’.